Header Ads Widget

Recent in Sports

test

DIT YASHIRIKI MAFUNZO YA KUWAONGEZEA VIJANA FURSA ZA AJIRA KUPITIA TEHAMA

    Na Mwandishi Wetu.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewataka vijana nchini kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kutangaza ujuzi na ubunifu wao, kujiajiri pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza, ikiwemo fursa zinazotarajiwa kutokana na ujio wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Wito huo umetolewa leo na Dkt. Maryam Ismail, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, aliyemwakilisha Mkurugenzi Prof. Stephen Oswald Maluka, wakati wa ufunguzi wa kitaifa wa mafunzo ya mradi wa majaribio unaolenga kuimarisha uwezo wa vijana na kuwaongezea fursa za ajira kupitia ujuzi wa kidigitali.

Mafunzo hayo pia yanalenga kupanua fursa za vijana katika kujifunza na kutumia teknolojia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

Tukio hilo limehusisha taasisi sita za elimu ya juu ambazo ni Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IAА), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dodoma.

Taasisi hizo zimeshiriki mafunzo hayo kwa njia ya mtandao, huku shughuli kuu za ufunguzi zikifanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Dkt. Mariam amesema ujuzi wa kidigitali si jambo la ziada katika elimu, bali ni sehemu muhimu ya ujuzi wa msingi unaohitajika katika maisha, ajira, biashara na ujasiriamali kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema vijana wanapaswa kutumia majukwaa ya kidigitali kutangaza uwezo, ubunifu na bidhaa zao ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuwa sehemu ya kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia pamoja na matukio makubwa ya kimataifa yanayofanyika nchini.

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Ezekiel Amri, amesema DIT ni taasisi iliyobobea katika masuala ya teknolojia ya habari na kwamba inajikita katika kuwapatia vijana ujuzi wa kidigitali utakaowasaidia kuboresha shughuli zao za kibiashara, ubunifu na utengenezaji wa maudhui.

Amri amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuongeza thamani katika shughuli zao na kufungua milango ya fursa mbalimbali.

Naye Mhadhiri kutoka Idara ya Kompyuta wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Phinian Mwalongo, amesema kupitia mafunzo hayo vijana watajengewa uwezo wa namna ya kuweka na kuwasilisha ujuzi wao kwenye kurasa zao za majukwaa ya kidigitali.

Amesema hatua hiyo itasaidia kurahisisha upatikanaji wao na waajiri, wateja na wadau mbalimbali wanaoweza kuhitaji ujuzi na huduma wanazozitoa.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya kidigitali katika kujitangaza, kujiajiri, kubuni bidhaa na huduma pamoja na kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia uchumi wa kidigitali.



















DIT YASHIRIKI MAFUNZO YA KUWAONGEZEA VIJANA FURSA ZA AJIRA KUPITIA TEHAMA DIT YASHIRIKI MAFUNZO YA KUWAONGEZEA VIJANA FURSA ZA AJIRA KUPITIA TEHAMA Reviewed by Adery Masta on September 21, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.