Na Mwandishi Wetu.
Katika hatua nyingine muhimu ya kukuza rasilimali watu na kuimarisha ubunifu wa kiteknolojia nchini, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imepeleka wanafunzi 30 wa fani ya Uhandisi Umeme kwenda nchini China kwa ajili ya programu ya kubadilishana ujuzi wa kitaaluma.
Wanafunzi hao wameondoka Mei 14, 2026 kuelekea Chuo cha Cho-Ching, ambapo watasoma kwa muhula mzima wakishirikiana na wenzao wa China. Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa kati ya DIT na chuo hicho cha China, yakilenga kubadilishana maarifa, teknolojia na uzoefu wa kimataifa.Akizungumza kabla ya safari hiyo, Naibu Mkuu wa DIT, Profesa Ezekiel Amri, aliwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuzingatia nidhamu, kujituma katika masomo yao na kutumia vyema fursa hiyo adhimu. Alisisitiza kuwa China ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kwa kasi katika ubunifu wa teknolojia na miundombinu, hivyo wanafunzi hao wanatarajiwa kurejea na maarifa yatakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali nchini.
“Fursa hii si ya kawaida. Taifa linawategemea mjifunze kwa bidii, mpate ujuzi wa kisasa na mje muongeze thamani katika sekta za viwanda, nishati na teknolojia kwa ujumla,” alisisitiza Prof. Amri.Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uhandisi Umeme, Dkt. Mwaka, alieleza kuwa programu hiyo ni daraja muhimu la kuwajengea wanafunzi uwezo wa kimataifa (global competence), unaojumuisha maarifa ya vitendo, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na uelewa wa mifumo ya uzalishaji wa viwandani ya kiwango cha juu. Aliongeza kuwa wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza mbinu za ubunifu (innovation techniques), kufanya kazi kwenye maabara za kisasa, na kushiriki miradi ya pamoja na wanafunzi wa China.
“Tunategemea kuona matokeo chanya kupitia ubunifu watakaokuja nao, hasa katika maeneo ya nishati mbadala, automatisering ya mifumo na suluhisho za kiteknolojia zinazokidhi mazingira ya Tanzania,” alisema Dkt. Mwaka.Nao wanafunzi, wakiwemo Barnaba Madilisha, walieleza furaha yao kwa kupata nafasi hiyo adhimu, wakiahidi kuitumia vyema kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla. Walitoa wito kwa serikali na taasisi kuendelea kupanua programu kama hizi ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
“Ni nafasi ya kipekee sana. Tunaamini tutapata ujuzi mkubwa na tutakaporudi tutakuwa sehemu ya mabadiliko ya kweli nchini,” alisema Barnaba.Ushirikiano kati ya DIT na Chuo cha Cho-Ching unatajwa kuwa mfano bora wa diplomasia ya elimu (education diplomacy), ambapo mataifa yanatumia elimu kama nyenzo ya kujenga mahusiano ya kudumu na maendeleo ya pamoja. Kupitia MoU hiyo, pande zote mbili zinanufaika kwa kubadilishana wanafunzi, wahadhiri, pamoja na tafiti za pamoja zinazolenga maendeleo ya teknolojia na viwanda.Hatua hii inaakisi dhamira ya Tanzania ya kuwekeza katika elimu ya juu yenye mwelekeo wa kimataifa, huku ikiandaa kizazi cha wataalamu watakaoweza kushindana katika soko la dunia na kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia sayansi na teknolojia.
Reviewed by Adery Masta
on
May 14, 2026
Rating:









No comments: