Header Ads Widget

Recent in Sports

test

DIT NA CEBOT WAINGIA MAKUBALIANO

 Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na taasisi ya Council Exchange Board of Trade (CEBOT) ya Marekani leo Machi 23, 2026, hatua inayotarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimataifa katika elimu ya ufundi, utafiti na ubunifu.

Mkuu wa taasisi hiyo, Prof. Preksedis Ndomba, amesema makubaliano hayo ni fursa kubwa kwa DIT kupanua wigo wa ushirikiano wa kitaaluma na kiviwanda, akibainisha kuwa CEBOT inawakilisha zaidi ya makampuni 65,000, huku zaidi ya makampuni 2,000 tayari yameonesha nia ya kushirikiana na DIT. Amesema hatua hiyo inaashiria imani kubwa ya wadau wa kimataifa kwa uwezo wa taasisi hiyo katika kuendeleza teknolojia na ubunifu.



Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano huo, DIT kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) itaongoza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kisayansi na kiteknolojia nchini, ikilenga kukuza tafiti zenye tija na suluhisho bunifu kwa maendeleo ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Prof. Ndomba, wadau hao wa kimataifa wamevutiwa na ubora wa ufundishaji na tafiti zinazofanywa na DIT, pamoja na fursa zilizopo katika kuendeleza biashara kupitia teknolojia bunifu zinazozalishwa na taasisi hiyo.

Kupitia makubaliano hayo, DIT inalenga kuimarisha ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi kwa kukuza ubadilishanaji wa uzoefu, utaalamu na rasilimali za kufundishia na kujifunzia kati ya pande hizo mbili.

Ushirikiano huo pia unaendana na juhudi za Tanzania katika kujenga uchumi wa kidigitali pamoja na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kwa kulenga kukuza rasilimali watu, kuendeleza teknolojia na kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kimataifa.

DIT inaendelea kutekeleza mfumo wa Mafunzo na Elimu Kulingana na Uwezo (CBET), unaolenga kuzalisha wahandisi, mafundi na wataalamu wabunifu wenye ujuzi wa vitendo, wanaoweza kujiajiri na kuajiriwa, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda na uchumi wa nchi.








DIT NA CEBOT WAINGIA MAKUBALIANO DIT NA CEBOT WAINGIA MAKUBALIANO Reviewed by Adery Masta on March 23, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.