KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza TBS kwa kazi nzuri yenye weledi hususani katika kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 18,2024 Jijini Dar es Salaam, mara baada ya kamati hiyo kutembelea TBS na kujionea uwekezaji ulivyofanyika hususani kwenye jengo la maabara ambapo wameipongeza Serikali kwa uwekezaji walioufanya.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deus Sangu (Mb) amesema Serikali ilifanya jambo la muhimu kuwekeza fedha katika kuboresha miundombinu ya jengo la maabara ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya upimaji wa sampuli na uhakiki wa vifaa.
"Serikali imewekeza takribani bilioni 20 kwenye ujenzi wa jengo la kisasa la Maabara ya TBS Dar es Salaam pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 500 ambavyo vinatumika katika kupima na kuhifadhi sampuli za chakula pamoja na vipodozi". Amesema
Pamoja na hayo Mhe.Sangu amesema wataendelea kuhimiza uwajibikaji kwa Serikali katika taasisi hiyo kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu yao ili
kumlinda mlaji wa mwisho.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu (TBS), Dkt. Athuman Ngenya amewasisitizia wafanyabiashara kuhakikisha wanafuata taratibu za kuingiza bidhaa nchini na kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango ili kuepuka hasara ambazo zinaweza kujitokeza kama kugharamia uteketezwaji au kuzirudisha zilikotoka.
Amesema TBS inajitahidi kutoa elimu ya masuala ya usalama na ubora wa chakula na vipodozi kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali kama kupitia mitandao ya kijamii, kampeni za elimu kwa umma, vikao na wadau, vyombo vya habari na tovuti ya taasisi.
“Wafanyabiashara kabla hawajaagiza vipodozi nje ya nchi wanatakiwa kupita kwenye tovuti yetu waone vipi ambavyo vinakubalika na vipi ambavyo havikubaliki ili kutopata hasara. “ Amesema
PIC YATEMBELEA MAABARA ZA TBS, YAFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WAKE
Reviewed by Adery Masta
on
May 18, 2024
Rating:
No comments: