MWANAHARAKATI huru, Bihimba Mpaya, ametoa msaada wa fedha kwa Taasisi ya Jamiiyatul Akhlaaqul Islaam (JAI), kwa ajili ya kuhudumia chakula wagonjwa wanaohitaji msaada katika Hospitali ya Wilaya ya Kivule, jijini Dar es Salaam.
Akitoa msaada huo kwa uongozi wa JAI, leo tarehe 22 Disemba 2023, Bihimba amesema kiasi hicho cha fedha kitasaidia kutoa msaada wa chakula kwa wagonjwa hasa kina mama wajawazito wanaojifungua, kwa muda wa wiki moja.
“Hii taasisi imejitokeza kupambana na changamoto za wagonjwa katika hospitali zetu, leo nimekuja kuisaidia kwa kuipa fedha ili ziweze kusaidia wagonjwa wasiojiweza. Kuna neno linasema ukitenda wema utalipwa wema, ukifanya ubaya utalipwa ubaya, hivyo nimeamua kutenda wema,” amesema Bihimba .Mwanaharakati huyo amesema “eo nawakabidhi fedha hizi kwa ajili ya kuandaa chakula kwa wagonjwa wanaokuja hospitali ya wilaya ya Kivule ambayo itasaidia wiki nzima.”
Mbali na kutoa msaada huo, Bihimba ameiomba Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itenge fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara inayokwenda hospitalini hapo, ili kuwaondolea wagonjwa adha ya usafiri.
“Naishukuru Serikali kwa kujenga hospitali hii ya Kivule, lakini ina changamoto kubwa ya barabara inayofika hospitalini hivyo wagonjwa wanashindwa kufika kwa wakati sababu ni mbovu. Namuomba Rais Samia aingilie kati ili barabara hii ikarabatiwe kwa kiwango cha changarawe wakati wanasubiri lami kwa kuwa inatesa wananchi hata wajawazito wengine wanalazimika kujifungua njiani,” amesema Bihimba.Mratibu wa JAI, Said Mshaka, amemshukuru Bihimba kwa kutoa msaada huo akisema utasaidia kutekeleza majumu yao ya kuhudumia wagonjwa.
Mshaka amesema JAI ilianzishwa 2014 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa ambao hawana ndugu au wasiokuwa na uwezo walioko hospitalini na majumbani kwa kuwapa vyakula, kuwanunulia dawa na vifaa vya matibabu, pamoja na kuwalipia vipimo vya magonjwa mbalimbali.
Mbali na kusaidia wagonjwa, Mshaka amesema JAI inafanya kazi ya kuhamasisha jamii kuchangia damu, kutembelea wafungwa na mahabusu gerezani pamoja na kuwapa mahitaji maalum na kuzika maiti zisizokuwa na ndugu.
No comments: