Na Mwandishi Wetu.
Inaelezwa kuwa, wabunifu wa Tanzania ni wazuri lakini wanahitaji kutangazwa ili waonekane na watu wenye kampuni kubwa duniani waweze kuwekeza katika uzalishaji.
Hayo yanaelezwa na Meneja Usimamizi na Uhawilishaji Teknolojia kutoka Tume ya Sayansi na Teknojojia (COSTECH), Erasto Mlyuka katika ufunguzi wa semina ya siku tatu inayofanyika katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa watumishi 45 wa DIT ili kuwajengea uwezo na kuimarisha vituo vya teknolojia na ubunifu.
“Wabunifu wetu Tanzania ni wazuri lakini wanahitaji kutangazwa ili watu wenye fedha, wenye kampuni kubwa duniani waje kuwekeza kwenye bunifu zao,” anasema Erasto na kuwataka vijana kuwa na utamaduni wa kushirikiana na si kushindana katika ushindani wa kimataifa.
“Kama ni kushindana kuwe ni kwa tija, kama mbunifu mmoja ana kitu cha kipekee na mwingine ana kitu cha kipekee mnaweza kuja pamoja na kupata mtaji kufanya kitu pamoja,” amesema.
Hata hivyo Erasto amesema nchi iko mahali pazuri kwani kwa mujibu wa takwimu za ripoti ya mwaka huu kuna kampuni changa zaidi ya 600, amesema “tunaamini kila kampuni inapambana kuhakikisha inapata mtaji ili bunifu ziwafikie walaji na tunaamini tutaendelea kuonekana kimataifa.”
Mratibu wa Utafiti, Ubunifu na Machapisho wa DIT, Dkt. Daudi Simbeye amesema semina hiyo ina lengo la kuboresha utafiti na bunifu zisiweze kuibuwa au kuzalishwa na watu wengine ndani na nje ya nchi, kupitia semina hiyo iliyoratibiwa kwa kushirikiana na COSTECH, walimu na wanafunzi wataweza kulinda bunifu zao.
"Hapa kwetu DIT tumejikita zaidi katika kufundisha na kutoa ushauri wa kitaalam, pia tumekua tukifanya bunifu mbalimbali lakini changamoto ni namna gani ya kulinda bunifu zetu, semina hii inakwenda kutuongoza nini cha kufanya katika changamoto hiyo,” amesema.
"Moja ya faida ya semina hii ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ikiwa ni zile zinazotokana na bunifu zetu ziweze kuwa bora na zishindane kitaifa na kimataifa na ziweze kuleta tija na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla," amesema Dkt. Simbeye.
Ameshauri serikali kuendelea kuzipa taasisi vifaa vya kufundishia vya kutosha na vya kisasa ili ziendelee kuzalisha vijana wenye tija na taasisi hizo ziendee kusaidia kutatua changamoto katika jamii.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia dar es Salaam, Prof. Preksedis Ndomba amepongeza COSTECH kuendesha mafunzo hayo ambayo yatasaidia wabunifu kunufaika na bunifu zao.
“Ni matarajio yangu baada ya semina hii wataalamu wetu watakuja na mpango kazi bora wa kubiasharisha bunifu zetu lakini pia bunifu na teknolojia nyingi zaidi zitabiasharishwa,” amesema Prof. Ndomba.
Mwalimu Idara ya Uhandisi Mitambo, Gerutu Bosinge ameshukuru semina hiyo, anasema itasaidia namna ya wabunifu kumiliki bunifu zao na kujenga uwezo wa walimu lakini pia walimu kujenga uwezo wa wanafunzi wao.
"Hii itatusaidia sisi kama walimu lakini pia wanafunzi wetu katika kumiliki bunifu zao na kuzifikisha bunifu zetu sokoni, kama nchi itasaidia kupunguza gharama ya kuagiza vitu ambavyo tunaweza kutengeneza sisi wenyewe," amesema Gerutu.
No comments: