Na Mwandishi Wetu.
Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) leo imefanya ukaguzi wa hosteli za wanafunzi katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam kukagua kazi ya ukarabati wa majengo hayo ikiendelea ambapo Meneja wa Mradi huo ameahidi kufikia mwezi Oktoba kazi hiyo itakua imekamilika.
Ukarabati huo unafanyika baada ya serikali kutoa Sh bilioni 2.7 kwaajili ya ukarabati wa majengo ya hosteli za wanafunzi zikizopo Kampasi ya Dar es Salaam na jengo lililopo Chang'ombe wilaya ya Temeke.
Akizungumza katika ziara hiyo, Meneja wa Mradi wa Ukarabati, Mhandisi Dkt. Johnson Malisa amesema wanatarajia kazi hiyo kukamilika kabla wanafunzi hawajafungua chuo.
"Tunajitahidi kuhakikisha kazi hii ikamilike kabla wanafunzi hawajafungua chuo ili watakaporudi wakute mazingira ni mazuri, waishi vizuri na kusoma kwa ufasaha bila usumbufu," amesema.Amesema kazi ya ukarabati inafanyika kwa utaratibu wa kutumia mafundi wa kawaida wakisimamiwa na wataalamu wa DIT ambapo kazi inayofanyika ni ukarabati wa vyoo, uwekaji wa mifumo mipya ya umeme na maji, makabati mapya na ukarabati wa majengo kwa ujumla.
Ameiambia Menejimenti hiyo kuwa katika kazi hiyo baadhi ya wanafunzi watapata fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika dhana ya Taasisi hiyo 'Teaching Factory'.Aidha, ameahidi Menejimenti ya DIT kuwa ukarabati huo utafanyika chini ya usimamizi wa hali ya juu ili thamani ya fedha iliyotolewa na serikali ionekane.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Taasisi hiyo Utawala na Fedha, Profesa Najat Mohammed ameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha za kukarabati wa hosteli hizo kwani zilikua zimechoka kwasababu ni za muda mrefu."Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha hizi, ni kweli majengo haya yalikua yamechoka sana na miundombinu ya umeme na maji imechoka mno, baada ya kukamilika ukarabati wanafunzi watasoma vizuri hasa wanafunzi wa kike," amesema.
Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Preksedis Ndomba amesisitiza kuzingatia muda uliopangwa ili kuhakikisha wanafunzi wanapofungua chuo wakute mazingira mazuri ya kusomea. Aidha amesisitiza pia usimamizi mzuri wa ukarabati huo ili fedha iliyotolewa na serikali itumike ilivuopangwa n itatue changamoto iliyokuwepo.
No comments: