Header Ads Widget

Recent in Sports

test

BENKI YA TCB WAFANYA MAZUNGUMZO NA SPIKA WA BUNGE

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania ( TCB ) Bw. Adam Mihayo akisalimiana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson alipomtembelea mapema Leo hii , Pembeni ni Mkurugenzi wa Biashara za Wateja wadogo na wa Kati wa Benki hiyo Bi. Lilian Mtali.

Na Adery Masta.

KATIKA jitihada za kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za kifedha na mihimili ya Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Bw. Adam Mihayo, amemtembelea na kuzungumza na Spika wa Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Tulia Ackson.

Bw. Mihayo ameambatana na Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo Bi. Lilian Mtali, katika ziara hiyo ambayo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Benki ya TCB na Bunge la Tanzania katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.

Mazungumzo na kiongozi huyo wa Bunge linaloundwa na wabunge 393 kutoka majimbo 239 yamejikita katika masuala nyeti yanayohusu majimbo mbalimbali katika jitihada za kuendelea kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati.

Wakitambua mchango mkubwa wa kundi hili katika ukuaji uchumi na uzalishaji wa ajira mpya, mazungumzo yao yamejikita katika kuanzisha mpango wa ruzuku, mikopo ya riba nafuu, na misamaha ya kodi kwa wajasiriamali. 

Miradi hii itasaidia kukuza na kuchochea mazingira ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na biashara zao.

“Lengo letu sio kutoa jibu moja kwa nchi nzima.


 Huwezi kuwa na suluhisho moja kwa watu wote, ndiyo maana ni muhimu kuwasikiliza wadau wengi iwezekanavyo. 


Njia hii itatusaidia kutoa majibu yatakayokidhi mahitaji ya wajasiriamali kulingana maeneo wanayoishi hata wale walioko vijijini,” amesema Bw. Mihayo.


Kwa upande wake, Mheshimiwa Tulia Ackson amebainisha umuhimu wa ushirikiano huo na kusisitiza wajibu wa Bunge katika kutunga sera zinazowezesha maendeleo ya wajasiriamali na kuhakikisha kwamba biashara zao zinapata rasilimali zinazohitajika ili kukua.

 “Maendeleo ya wajasiriamali ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa taifa letu, kupitia ushirikiano huu na Benki ya TCB, tunaweza kutengeneza mazingira yatakayowezesha ukuaji wa biashara,“ amesema.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa azimio la ushirikiano wa pamoja na kuendelea kubuni nyanja mbalimbali za ushirikiano lengo likiwa kuinua sekta ya wajasiriamali nchini. 


Ushirikiano huu unategemewa kufungua miradi mbalimbali itakayosaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.

BENKI YA TCB WAFANYA MAZUNGUMZO NA SPIKA WA BUNGE BENKI YA TCB WAFANYA MAZUNGUMZO NA SPIKA WA BUNGE Reviewed by Adery Masta on August 15, 2024 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.