Na Mwandishi Wetu.
TAASISI Maalum ya kifedha inayotoa mikopo ya muda mrefu kwa benki na taasisi za fedha kwa lengo la benki hizo na taasisi kutoa mikopo ya nyumba ya muda mrefu kwa wateja wao (TMRC) imeikaribisha benki ya ABSA Tanzania kama mwanahisa wake mpya.
Benki ya Absa imejiunga na TMRC kama mbia wa 19 kufuatia uwekezaji wa mtaji wa shilingi bilioni 1.62 ambapo benki hiyo inaungana na wanahisa wengine wa TMRC wa taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na CRDB Bamk Plc, Benki ya NMB Plc, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) pamoja na benki na taasisi zingine za kifedha.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Bw. Oscar Mgaya amesema kuwa benki ya Absa kujiunga na TMRC, benki hiyo itaweza kupata fedha nyingi zaidi kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba kutoka TMRC kama sehemu ya mkakati wake wa kukuza biashara yake kupitia utoaji wa mikopo ya nyumba.
Aidha amesema kuwa wanafurahi kuona benki nyingi zinajiunga na TMRC kwani kumekuwa na taasisi nyingi zaidi zikitoa mikopo ya nyumba .
"Mpaka sasa Tanzania kuna taasisi za fedha 31 ambazo zinatoa mikopo ya nyumba, leo Benki ya Absa amejiunga na TMRC na kufikia wanahisa 19, hivyo tunategemea taasisi nyingi kujiunga na TMRC na tunaendelea kuwashawishi wafanye hivyo". Amesema Bw. Mgaya.
Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Bw. Obedi Laiser amesema kuwa wamewekeza Bilioni 1.6 kwa TMRC kwaajili ya kuboresha maisha ya watanzania kwa kuwapatia mikopo ya nyumba bora za makazi kwa bei nafuu.
Amesema kuwa azma yao kuu ni kuiwezesha Afrika ya kesho kwaajili ya kuboresha maisha ya watu ambao ndio walengwa kwa kubadilisha maisha yao kupitia mikopo ya nyumba.
Kutoka kushoto, Mwenyekiti wa Bodi TMRC, Bw. Theobald Sabi, Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Bw. Oscar Mgaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Bw. Obedi Laiser pamoja na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi Benki ya Absa, Bw. Richard Magongo wakikabidhiana hundi ya shilingi bilioni 1.62 ambazo zimetolewa na Benki ya Absa Tanzania kama mwanahisa mpya wa TMRC. Hafla hiyo imefanyika leo Februari 5,2024 Jijini Dar es Salaam.
No comments: