SERIKALI imepongeza maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri wa Bidhaa za Ngozi na Teknolojia zinazoshabihiana (CELPAT) katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza ambapo mpaka sasa mradi huo wa ujenzi wa Kituo hicho umefikia asilimia 20.
Mradi huo unajengwa kwa ufadhili wa Serikali kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa EASTRIP ambao unatekelezwa katika nchi 5 Afrika, kwa Tanzania vyuo vinavyonufaika ni DIT Kampasi Kuu ya Dar es Salaam, DIT Kampasi ya Mwanza, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).Pongezi hizo zilitolewa na Mratibu wa Mradi wa EASTRIP Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Noel Mbonde wakati wa ziara ya siku moja ya kukagua mradi huo.
‘’Mradi huu mpaka sasa umefika hatua nzuri sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inasisitiza sana mafunzo ya ufundi kwa vijana wetu ili waweze kujiajiri na kuajirika’’ amesema Dkt. Mbonde na kuongeza mradi huo kwa DIT Mwanza ukikamilika utasaidia kutekeleza Tanzania ya Viwanda.Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Baraza la Vyuo Vikuu Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA) Prof. Idris Ahamada Rai ameshauri mkandarasi kuongeza kasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
"Mradi unaenda vizuri na sisi tumeridhika na kazi inayofanyika, vifaa anavyotumia mkandarasi, lakini tunashauri aongeze kasi kuendana na muda bila kuacha ubora.... ujenzi lazima uzingatie ubora," amesema.Aidha, amesema kamati hiyo inapita katika vyuo vyote ambavyo vinatekeleza mradi wa EASTRIP kuona maendeleo ya mradi lakini pia kushauri mambo mbalimbali ya kitaalamu.
Mratibu wa mradi CELPAT, Dkt. Albert Mmari amesema mradi huo unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2024. Alisema mradi huo una awamu mbili ambapo awamu ya kwanza mradi utagharimu Sh bilioni 19 na awamu ya pili utatumia Sh bilioni 7.1.Amesema mradi huo ukikamilika utaongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 200 mpaka wanafunzi 2000, kuongeza ajira kwa vijana na utasaidia kuleta chachu katika uzalishaji wa bidhaa za ngazi.
"Zao la ngozi halijapata msukumo wa kutosha lakini kupitia mradi huo viwanda vya ngozi vitaanzishwa," amesema Dkt. Mmari.Mkandarasi wa kampuni ya Comfix inayojenga majengo hayo, Allen Magoma alisema mradi huo ulianza Septemba 2022 na unatarajiwa kukamilika kwa mwaka mmoja, ameahidi kufanya kazi usiku na mchana na kuzingatia ubora.
No comments: