Na Mwandishi Wetu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe ameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kutekeleza vizuri Mradi wa EASTRIP ambao utaanzisha Kituo cha Kikanda cha Umahiri wa TEHAMA (RAFIC) katika Kamppasi Kuu ya Dar es Salaam.
Prof. Mdoe ametoa pongezi hizo leo alipotembelea DIT kupata taarifa na kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika Februari mwakani."Niwapongeze DIT kwa utekelezaji wa mradi huu, vigezo vinavyopimwa kwa upatikanaji wa fedha za mradi, mnafanya vizuri sana," amesema Prof. Mdoe.Aidha, Prof. Mdoe amesisitiza kazi ya ujenzi wa kituo hicho isimamiwe kwa ukaribu na mara kwa mara ili mkandarasi amalize kwa haraka lakini pia kazi ifanyike kwa ubora.
"Serikali inataka kuona thamani ya pesa ikionekana katika mradi huu, kazi ifanyike kwa haraka lakini kwa umakini mkubwa na sio kwenda kwa kasi tu," amesema.
Amemtaka Mratibu wa Mradi huo kuhakikisha kazi ambazo hazijakamilika zifanyike mapema kabla mradi haujapita muda wake wa kupimwa ili fedha yote iliyotakiwa kutolewa ipatikane kwa asilimia 100 ili ujenzi ukamilike.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ilipata fedha ya mkopo wa takribani USD 16.25 Milioni Mkopo ambao ni wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kuwezesha kuanzisha Kituo cha Umahiri wa Tehama Afrika Mashariki. DIT pia ilifanikiwa kupata mradi mwingine wa USD 16.25 Milioni wa kuanzisha Kituo cha Kikanda cha Umahiri wa Bidhaa za Ngozi kituo kitakachojengwa DIT Kampasi ya Mwanza.Mkataba wa ujenzi wa Kituo cha RAFIC umesainiwa Januari 10,2023 na unatarajiwa kukamilika Februari 2024.
No comments: